dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 26, 2015

Jukwaa la Wakristo lapinga Mahakama ya Kadhi kujadiliwa bungeni

Dar es Salaam. Wakati macho na masikio ya Watanzania wengi yakielekea mjini Dodoma kesho katika vikao vya Bunge vinayotarajia kujadili Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, Jukwaa la Wakristo nchini limeitaka Serikali isitishe kujadili marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislam ya mwaka 1964.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa hilo leo inasema Muswada huo unaolenga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi utasabisha kuvunjika kwa misingi ya Taifa hili kama lisilo la kibaguzi na kufungamana na dini yeyote.
Taarifa hiyo pia ilisema mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa yatakayokuwa na athari kubwa na nzito; kwani yanahoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini.
“Kama ambavyo tumesema mara nyingi, masuala yanayohusu imani za dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEC, Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa CPCT, Askofu Daniel Awet.
Kwa mujibu wa tamko hilo, Mahakama za Kadhi, pamoja na Mahakama za Wenyeji (Native Courts), zilizokuwepo wakati wa ukoloni zilifutwa na Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrates Courts Act) ya mwaka 1963 hivyo tangu wakati huo, mahakama hizi hazipo na hazitambuliwi na sheria yoyote. Hivyo, mapendekezo ya Muswada huu yakipitishwa ndiyo yatazianzisha.
“Kwa mapendekezo haya, Serikali inachukua jukumu la kuanzisha yenyewe taasisi za kidini kinyume na utaratibu wa kikatiba ambapo Serikali imekuwa haijishughulishi na uanzishwaji na uendeshaji wa taasisi za kidini. Hii ni kwa sababu Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu haikuanzisha mahakama au taasisi nyingine yoyote ya kusimamia Sheria hiyo bali iliweka utaratibu wa mahakama za kawaida kuitambua na kuisimamia Sheria hiyo.”
Tamko hilo linaeleza zaidi kuwa mapendekezo ya Muswada huo yanaleta sintofahamu kama mamlaka za mahakama za sasa za kusikiliza na kuamua masuala ya hadhi ya mtu, mirathi na ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu itaendelea kuwepo.
“Aidha mapendekezo ya Muswada huu yako kimya juu ya uhusiano wa Mahakama za Kadhi na mahakama za kawaida. Kwa mfano, haieleweki (haikuwekwa wazi) kama kutakuwa na utaratibu wa rufaa, marejeo na mapitio ya maamuzi ya mahakama hizo. Endapo, kwa mfano, mtu hataridhika na maamuzi ya Mahakama ya Kadhi, je, atakuwa na haki ya kukata rufaa? Kama atakuwa na haki hiyo, rufaa hiyo itapelekwa kwenye mahakama au chombo gani?”
“Mapendekezo hayo hayo, pamoja na kwamba wadaawa wataenda kwa hiari yao, yako kimya juu ya kesi zinazohusu Waislamu na watu wa imani nyingine. Na hata kwa wadaawa ambao ni Waislamu, ikiwa upande mmoja (tuseme wa Mdai) unakwenda kwa hiari ila upande mwingine (wa Mdaiwa) unataka shauri lisikilizwe na mahakama ya kawaida, Muswada hautoi jibu nini kifanyike.” 
Taarifa hiyo inasema pia kuwa suala hilo la Mahakama ya Kadhi lilikataliwa na Bunge Maalumu la Katiba wakati wa kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa hivyo  kushangazwa na suala hili kuibuka kwenye Muswada huu baada ya kuwa limekataliwa.
“Sisi viongozi wa Makanisa wanachama wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaamini kwamba sababu zilizopelekea kufutwa kwa mahakama hizi mwaka 1963; yaani, kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, bado ni halali na za msingi leo hii. Kwa sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri  kwamba Serikali iondoe Muswada huu Bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilo fungamana na dini,” inasema taarifa hiyo.

No comments :

Post a Comment