dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 26, 2015

Sitta, Lukuvi, Chiza wapigwa zengwe

  Wamo pia Simbachawene, Kilango, Dk. Mwakyembe aliliwa Uchukuzi.

Rais Jakaya Kikwete.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete juzi, yamekosolewa na wadau mbalimbali, wengi wakilalamikia kuondolewa kwa Dk. Harrison Mwakyembe, kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 
 Pia wametilia mashaka utendaji wa Samuel Sitta aliyehamishiwa Uchukuzi kutoka Ushirikiano wa Afrika Mashariki na William Lukuvi aliyehamishwa kutoka Ofisi ya waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakisema wizara hizo zina changamoto nyingi kulinganisha na uwezo wao wa utendaji.
 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Christopher Chiza, aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, nao wameelezwa kuwa hawakupaswa kuacha katika baraza hilo kutokana na utendaji usioridhisha. Yumo pia Anne Kilango aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango.Aliyekuwa Ofisa  Mwandamizi wa masuala ya Biokemia wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa Wakoti Nkya, ameyakosoa mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete ya kumuondoa Dk. 
 
Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi na kumhamishia Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.
 
Alisema kuwa  hayana tija kwa taifa kwa kuwa yanalenga kumpunguza kasi baada ya kutibua ‘madudu’ Mamlaka ya Bandari (TPA), Shirika la Ndege nchini (ATCL) na Kampuni ya Reli (TRL).
 
“Mwakyembe ameondolewa kwa sababu aligusa mizizi ya matajiri wachache baada ya kuivuruga vuruga Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)ambayo imegeuzwa shamba la bibi na akaanza kuwashughulikia vigogo hao kwa kuwasimamisha kazi na wengine kuwafukuza…TRL nako alirejesha imani kwa wasafiri wa treni baada ya kufanya maboresho makubwa, lakini ukweli kwamba alitoboa mirija ya wajanja, ndiyo maana kapelekwa Afrika ya Mashariki,” alisema Profesa Nkya.
 
Profesa Nkya alisema kumuondoa Mwakyembe katika wizara hiyo kutarejesha nyuma matumaini yaliyokuwa yameonekana ya kulifufua upya Shirika la Reli nchini ambalo lilikuwa limetumbukia shimoni kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo uduni wa miundo mbinu yake, kufa kwa mitambo na kuziua njia za reli za kikaanda.
 
MHADHIRI IoU
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Iringa (IoU), Emanuel Damalo, alisema kwa mabadiliko hayo, Watanzania wasitegemee mashirika kama ATCL na viwanja vya ndege vilivyokuwa vikisumbuliwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya huku kukiwa na juhudi za makusudi za kuyaokoa yasiingie shimoni, zitaendelea kwa kuwa suala la uzalendo ni la mtu binafsi.
 
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi, alisema mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri hayana tija, kwa kuwa baadhi ya Wizara zitalegalega kutoa huduma kutokana na aina ya wanasiasa waliopewa kuziongoza kukosa utashi na uzalendo wa kweli wa kutumikia umma.
 
MWENYEKITI ASAs
Mwenyekiti wa Jumuiya za Wanataaluma Tanzania (ASAs), Paul Loisulie, alisema mabadiliko hayo ni ya Rais na washauri wake ndio wanaojua sababu za msingi za kuwaweka wahusika kwenye nafasi husika.
 
Hata hivyo, alisema baadhi ya watu akiwamo yeye amepokea kwa masikitiko uhamisho wa Dk. Mwakyembe kutoka Uchukuzi.
 
“Mnyonge apewe haki yake, alijitahidi sana pamoja na ugumu wa maeneo kama bandari, viwanja vya ndege (madawa ya kulevya), meli, reli, mabasi na malori... Maeneo yote haya yanagusa maslahi ya watu binafsi, sina uhakika wala matumaini kwamba anaeingia Uchukuzi atafanya vizuri zaidi ya anayeondoka,” alisema Loisulie na kuongeza kuwa wakati ukifika itajulikana.
 
Kuhusu Simbachawene kuchukua nafasi ya Prof. Muhongo, Mhadhiri huyo alisema anafaa kushika wizara hiyo kwa sasa.
 
Alisema mamlaka ya uteuzi haijakosea kumpa nafasi hiyo.  Hata hivyo, alisema lazima awe tayari kufanya kazi na watu wote hasa wabunge bila kujali itikadi za kisiasa na aepuke majigambo kama mtangulizi wake.
 
“Asikilize maoni ya watu na kuyafanyia kazi, unyenyekevu utamsaidia sana katika Wizara hii ngumu, Lukuvi (Willium) naye kwenye ardhi ana kibarua kigumu sana lakini akijipanga anaweza akafanya vizuri,” alisema.
 
MWENYEKITI THTU-UDOM
Naye Mwenyekiti wa chama wafanya kazi wa Elimu ya Juu tawi la Chuo Kikuu cha Dodoma (THTU-UDOM), Nashon Maisori, alisema  kwa jinsi Bunge lilivyo Rais anapata wakati ngumu wa kupata mawaziri kutokana na baraza lake kubadilishwamara kwa mara kufuatia mapungufu ya mawaziri.
 
“Mweshimiwa Rais amejikuta hana watu tena wa kuwapa uwaziri, inabidi tu sasa awekwe mtu kujaza nafasi na siyo lazima awe ana uwezo... Ila suala la Mwakyembe, mimi binafsi nimeshtuka sana, sikutarajia aondolewe Wizara ya Uchukuzi kwa sababu kwa mtizamo wangu alikuwa anafanya kazi nzuri sana,” alisema.
 
Aliongeza: “Hata kwenye mpira kocha humpumzisha mchezaji aliyechoka na siyo mchezaji anayetegemewa uwanjani. Kumpeleka huko Afrika Mashariki ni kupoteza mchapa kazi mzuri na kumpa kazi laini, mawaziri ambao walikuwa wakichapa kazi sana ni Magufuli na Mwakyembe tu wengine business as usual.” 
   
 CHAUMMA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Kayumbo Kabutari, alisema Baraza hilo ni la kivivu la bora wamalize salama inavyoelekea Kikwete amebanwa ndani ya chama chake na makundi ya urais yanayomhofia Mwakyembe ambaye ametengeneza jina kupitia Wizara ya Uchukuzi.
 
“Hivyo wamfiche Simbachawene ni mwendelezo wa kuficha uozo wa wizara husika hakuna asilolijua la kifisadi kwani alikuwa msaidizi wa karibu wa Muhongo upande wa nishati naibu waziri waliingia pamoja na Muhongo,” alisema Kabutari.
 
Kuhusu Lukuvi, alisema ameshindwa kutatua mgogoro mdogo wa ardhi wa Mamlaka ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) katika Manispaa ya Dodoma na wananchi, hivyo hataweza kushughulikia migogoro mikubwa ya ardhi nchi mzima,” alisema.
 
 “Hakuwatendea haki Watanzania kwa kumuondoa Dk. Mwakyembe Wizara ya Uchukuzi ambayo alikuwa anakwenda nayo vizuri na kumuingiza Sitta ambaye alikuwa Afrika Mashariki,” alisema Wachacha Peter, mkazi wa Mabatini, jijini Mwanza na kuongeza kuwa Rais Kikwete amerudisha nyuma maendeleo ya uchukuzi baada ya kumuondoa Dk. Mwakyembe na kumuingiza Sitta aliyekuwa Wizara ya Afrika Mashariki.
 
Alisema Wizara ya Uchukuzi ambayo inahitaji waziri mwenye kasi, inaweza kurudisha nyuma juhudi za wizara hiyo ambazo zilianza kuonyeshwa na Waziri Mwakyembe katika kufufua reli ya kati.
 
Hata hivyo, mkazi huyo alisema wizara nyingine zimefaanikiwa kupata watendaji wazuri ingawa wapo mawaziri ‘mizigo’ walioachwa na kupelekwa wizara nyingine.
 
Naye mdau wa siasa wa jijini Mwanza na mkazi wa Nyakato, Peter James, alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete hayana tija kwa Watanzania kutokana na baadhi ya wizara kiupelekewa mawaziri ‘mizigo’.
 
“Hakuna jipya alilofanya Kikwete zaidi ya kuzidi kuzipa wizara nyingine mizigo kutokana na kupelekewa watu ‘mizigo’...lakini kwa kipindi kilichobaki cha miezi sita hawatafanya lolote la maana,” alisema James.
 
Alisema kufanya uteuzi wa haraka haraka bila kuwafanya tathmini ya utendaji wao, Rais Kikwete anazidi kuwaongezea kero wananchi kwa kuwapo na mawaziri wasiowawajibikaji.
 
Hata hivyo, mkazi wa Buhongwa nje kidogo na Jiji la Mwanza, Christopher Chacha, alisema hashangazwi na mabadiliko hayo ya Kikwete kutokana na kushindwa kuwaondoa mawaziri kama Dk. Shukuru Kawambwa na Christopher Chiza.
 
JUKATA
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda, alisema babadiliko hayo yamefanyika kikiwa kimebaki kipindi kifupi cha serikali ya awamu ya nne kuondoka madarakani, hivyo  Watanzania wasitarajie mambo mapya.
 
“Hapo yamefanyika mabadiliko ya sura, hakuna jipya, kipindi kimebakia kifupi sana Watanzania wasitarajie jipya,” aliongeza.
 
DK. BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema zipo Wizara ambazo zinahitaji  utendaji wa hali ya juu na uzoefu katika kazi,  hususani Wizara ya Uchukuzi na Nishati ambazo alisema kwa uteuzi ulifanyika haamini kama kutakuwa na mabadiliko yoyote.
 
Alisema ameshangazwa na  mabadiliko katika Wizara ya Uchukuzi kwa  kuhamishwa  Dk. Mwakyembe  ambaye alionyesha mwanga kidogo  wa kushughulikia  changamoto zinazoikabili wizara hiyo nyeti.
 
“Nimeshaganzwa na uteuzi wa Dk. Mwakyembe kupelekwa Wizara ya Afrika Mashariki, wakati kuna matatizo makubwa ndani ya Wizara ya Uchukuzi ambayo alikuwa ameanza kuyashughulikia ambayo alipaswa aendelee ili ayamalize, ikiwamo suala la ATC, Bandari na kashfa zilizokuwa zinaendelea Uwanja wa Ndege,” alisema Dk. Bana na kuongeza:
 
“Ninavyoamini Wizara ya Afrika Mashariki anakwenda kupumzika tu kwa sababu haina kazi nyingi kama ilivyo ya Uchukuzi, ninashindwa kuelewa ni kwa nini ametolewa pale anajua Rais mwenyewe, lakini mimi naona Dk. Mwakyembe alifaa sana Uchukuzi.”
 
Aliongeza kuwa Sitta ni mtendaji mzuri, lakini kwa sababu Dk. Mwakyembe alikuwa ameanza kufanya kazi nzuri, ni vema angeendelea nayo ili kuhakikisha inakaa sawa.
 
Akizungumzia Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzi ya Ufundi, Anna Kilango, alisema haamini kama ataweza kuimudu wizara hiyo kwa kuwa uwezo wake ni mdogo.
 
Alisema hana imani kama Kilango ataweza kumshauri vizuri waziri wake  kwa kuwa ni mwanaharakati na kwamba  uharakati na kazi aliyopewa haviwezi kwenda pamoja.
 
Kuhusiana na Wiazara ya Nishati na Madini, ambayo amepewa Simbachawene, alisema Wizara hiyo ni muhimu na ambayo inahitaji mtu mzoefu na mchapakazi, lakini anaamini endapo atafanya kazi kwa bidii ataiweza.
 
DK. SLAA
 Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, alisema watanzania wasitarajie matumaini yoyote katika uteuzi huo.
 
Akimzungumzia Lukuvi, alisema wakati akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) alikuwa chanzo cha kukwamisha mchakato wa Katiba, hivyo kumpeleka katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ni kusababisha matatizo.
 
“Kwa ujumla hata  kwa hatua ambayo  Tanzania imefikia kwa sasa huwezi kutegemea kwamba yupo kiongozi yeyote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye atawaletea matumaini Watanzania, wote, ni matatizo matupu hakuna mwenye nafuu, eti unamtoa Waziri ambaye hata chama chake kinamwita mzigo unamhamishia Wizara nyingine,” alisema Dk. Slaa bila kuwataja.
 
Hata  hivyo, tangu mwaka juzi Katibu Mkuu wa CCM, Abdurlahman Kinana na Katibu Mwenezi, Nape Nnauye katika ziara zao za kuhimiza utekelezaji wa Ilani, wamekuwa wakiwataja kwa majina baadhi ya mawaziri kuwa ni mizigo. Miongoni mwao ni Chiza na Kawambwa.
 
Dk. Slaa alimtolea mfano Anna Kilango kwamba anadaiwa kuwa na kashfa ya kuuza kiwanda cha Tangawizi katika Jimbo la Same Mashariki, lakini anashangaa kuteuliwa kuongoza wizara muhimu.
 
PROF. BAREGU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema  uteuzi wa Rais umeonyesha wazi kuwa amekosa timu ya mawaziri wa kufanya nao kazi.
 
Alisema ni mara ya tano Rais anabadilisha Baraza la Mawaziri na kila anapofanya hivyo hakuna mabadiliko yeyote yanayoonekana.
 
“Mabadiliko haya ya Baraza la Mawaziri, yanaonyesha kuwa Rais amekosa timu ya Mawaziri wa kufanya nao kazi, hana  uwanja mpana  wa kumsaidia kupata watendaji, hii ni kwa sababu ya Katiba ambayo inamruhusu kuteua ndani ya Bunge tu wakati watendaji wengine wazuri wako nje ya Bunge,”  alisema Profesa Baregu.
 
Aliongeza: “Na ndiyo maana wananchi walipendekeza kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba Mawaziri wasiwe Wabunge, hii ingempa Rais wigo mpana na angepata watendaji wazuri, tofauti na ilivyo sasa, Rais anakosa watendaji kwa hiyo anakuwa anazunguka mle mle, anamteua Waziri anashindwa hapa, anamjaribu pengine  kwa sababu tu anakosa watu, na jambo hili  ni hatari. Kwa hiyo hata mimi siwezi kusema nani ataweza na nani atashindwa kwa sababu wengine tulisema wanaweza, lakini wameshindwa.”
 
DK. SEMBOJA
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji Semboja, aalisema ana imani na Sitta kutokana na uadilifu na utendaji wake kazi serikalini na kuwa lisema ili  Sitta afanye kazi kwa usahihi, anahitaji ushirikiano kati yake na watendaji wa wizara nzima.
 
“Mawaziri wengi wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa sababu ya kutopewa ushirikiano na watendaji, hali inayopelekea kuenguliwa nafasi zao,” alisema Dk. Semboja.
 
Kuhusu Simbachawene, alisema kinachotakiwa kufanyika ndani ya wizara hiyo ni kumpa ushirikiano ili aweze kutatua changamoto zilizomo na kufufua matumaini ya Watanzania.
 
Aidha, alisema hana wasiwasi na utendaji kazi wa Wasira kwa kuwa anafahamika kwa umakini wake kazini.
 
Aliongeza kuwa, bado ana wasiwasi na uteuzi wa Lukuvi kwa kuwa mara nyingi amekuwa akituhumiwa kwa utendaji usioridhisha.
 
“Natilia shaka utendaji wa kazi wa Lukuvi, ni bora Rais angemteua Naibu Waziri wake (Angela Kairuki) kuchukua nafasi, hapo nisingetilia shaka uteuzi uliofanyika,” alisema.
 
NYAKEKE WA TRAWU
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), alisema haungi mkono mabadiliko hayo hususan wale waliohamishwa kwenye wizara zao akiwamo Dk. Mwakyembe na Sitta aliyepelekwa kuchukua nafasi yake.
 
Alisema kubadilishwa kwa mawaziri wenye utendaji mzuri kama Dk. Mwakyembe kunarudisha nyuma utendaji na maendeleo ya wizara husika ambayo yalikuwa yameanza kuonekana na kwamba kwa kuwa uchaguzi mkuu umekaribia, ingekuwa vizuri kuwaacha katika wizara zao.
 
Kubadilishwa kwa Baraza hilo la Mawaziri kumetoka na Waziri aliyekuwa anaiongoza Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kufutwa kazi kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow. Imeandikwa na Godfrey Mushi, Moshi; Augusta Njoji,Dodoma; Daniel Mkate, Mwanza; Christina Mwakangale, Elizabeth Zaya na Hussein Ndubikole, Dar.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment