dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, May 25, 2015

Dk. Migiro azua hofu Chuo Kikuu Huria.

Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk. Asha-Rose Migiro.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk. Asha-Rose Migiro (pichani), ameshushiwa tuhuma nzito za kurudisha nyuma maendeleo ya chuo hicho kutokana na hatua yake ya kutomtangaza makamu mkuu mpya wa chuo hicho kuziba nafasi iliyoachwa na Profesa Tolly Mbwette aliyestaafu mwezi uliopita.
 
Hivi sasa, nafasi ya makamu wa chuo hicho inakaimiwa na Profesa Elifas Bisanda. Hata hivyo, ilielezwa na baadhi ya watumishi kuwa kuna hofu kubwa ya kurudi nyuma kitaaluma kwani baadhi ya mambo hayafanyiki vizuri kutokana na kukosekana kwa mrithi rasmi wa Mbwette.
 
Aidha, ilielezwa zaidi kuwa mchakato wa kumpata makamu mpya wa chuo hicho ulishaanza Aprili, 2014 na mapendekezo yalishafikishwa kwa Dk. Migiro, lakini mkuu huyo ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba bado anasita kumtangaza mrithi wa Mbwette kwa sababu anazozijua yeye.
 
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2015, Mkuu wa Chuo ndiye mwenye mamlaka ya kuteua Makamu Mkuu wa Chuo.“Kwakweli hofu imetanda. Mambo yameanza kwenda kombo... kuna maamuzi makubwa yenye manufaa kwa chuo yanashindwa kufanyika kwa sababu ya kukosekana kwa makamu mkuu wa chuo,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa chuo hicho chenye matawi nchini kote na pia kikiwa pekee chenye matawi katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Namibia na Malawi.
 
Inadaiwa kuwa hivi sasa, tayari baadhi ya wahadhiri wanafikiria kuhamia vyuo vingine kwa sababu mambo mengi yamesimama katika kipindi hiki cha kukosekana kwa makamu mkuu wa chuo.
 
“Kinachotushangaza ni huu ukimya unaoashiria picha mbaya kuwa labda chuo kinakosa watu wenye sifa. Kila mmoja anajua kuwa vetting (mchakato wa kuwapata wateule) ilishafanyika kwa mwaka mzima na majina alishapewa... sasa sijui (Dk. Migiro) anakwama wapi,” kilieleza chanzo kimoja kutoka chuoni hapo. 
 
Taarifa zaidi zilidai kuwa Dk. Migiro ana mtu wake ambaye siyo miongoni mwa majina aliyopewa na ndiyo maana anasita kutumia mamlaka yake ya kumtangaza makamu mkuu wa OUT, kama anavyopaswa kufanya kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005.
 
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi wa OUT walieleza kuwa miongoni mwa athari za kutokuwapo kwa makamu mkuu rasmi wa chuo chao ni pamoja na kutoagwa kwa mkuu aliyemaliza muda wake (Prof. Mbwette) kwani kwa kawaida jambo hilo hufanyika baada ya kutangazwa kwa makamu mpya.
 
“Na athari kubwa zaidi ni matumizi mabaya ya rasilimali za chuo. Hivi sasa kuna wakubwa husafiri kila mara na hakuna wa kuwazuia kwa sababu aliye madarakani (kaimu makamu mkuu) hawezi kufanya maamuzi magumu... na hili liko wazi tu kwa sababu yeye (kaimu makamu) hana uhakika wa kuendelea kubaki katika nafasi hiyo. Hajui pengine huyo atakayemuadhibu leo ndiye kesho anakuwa bosi wake,” chanzo kingine kiliongeza.
 
Akizungumzia hali hiyo ya kukosekana kwa makamu mkuu wa OUT, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela, alisema suala hilo halipo tena wizarani kwao na hivyo aulizwe mkuu wa chuo hicho, Dk. Migiro.
 
“Hivi sasa jambo hilo halipo chini ya Waziri wa Elimu...lipo kwa Mkuu wa Chuo,” alisema Kilango na kuongeza kuwa mchakato ulishafanyika na Mkuu wa Chuo (Dk. Migiro) alishapewa majina matatu ya watu wanaofaa kushika nafasi hiyo ili amtangaze mmoja kati ya hao kumrithi makamu aliyemaliza muda wake. 
 
 Kufuatia uthibitisho wa Naibu Waziri wa Elimu kuwa majina ya wateuliwa wa nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria yalishakabidhiwa kwa mkuu wa chuo hicho, NIPASHE ilimtafuta Dk. Migiro ili kupata maelezo yake. Baadhi ya maswali yalikuwa na nia ya kupata maelezo yake kuhusiana na madai kwamba ana mtu wake hayumo kwenye orodha aliyopewa na ndiyo maana anasita kutoa uamuzi na pia, kujua ni kwa vipi anasumbuliwa na maamuzi hayo wakati naye amekuwa akitajwa kuwa anafaa siku moja kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa nchi hii na hivyo kutakiwa afanye maamuzi magumu zaidi ya hayo ya kutangaza jina la makamu mkuu wa chuo.
 
Hata hivyo, Dk. Migiro alimjibu mwandishi kwa ufupi akisema: “No comment” (sina cha kueleza).
 
Chuo Kikuu Huria kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 17 ya 1992, mkuu wake wa kwanza akiwa Waziri Mkuu Mstaafu, John Samuel Malecela, aliyedumu kuanzia mwaka 1992 hadi aliporithiwa na Dk. Migiro mwaka 2013. Makamu mkuu wa kwanza wa OUT alikuwa Profesa Geofrey Mmari.  
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment