dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, July 24, 2015

Kama akiwa Rais Nani atamfunga ‘gavana’ Magufuli?


NIANZE kwa kuwaomba radhi wasomaji wangu kwa kutoweka ghafla, na kwa muda mrefu katika safu hii. Ukweli ni kwamba muda wote huo nilikuwa kijijini nikimuuguza baba yangu mzazi ambaye hata hivyo alifariki dunia. Baada ya mazishi niliamua kupumzika hukohuko kijijini.
Nakumbuka makala yangu ya mwisho kwenye safu hii ilikuwa na kichwa kinachosomeka; Lowassa si muumini wa ‘Janteloven’, anatufaa urais? Ilichapwa kwenye toleo Na. 380 la Novemba 2014.
Makala hiyo, ambayo kimsingi ilihitimisha kuwa Lowassa hafai kuwa rais wetu, ilihusishwa na baadhi ya wasomaji wangu (kwa sms nyingi walizonitumia) na kutoweka kwangu ghafla kuandika katika safu hii.
Baadhi walinituhumu kuwa nilipewa pesa nyingi ili nisiendelee kuandika tena kuhusu Edward Lowassa, na ndiyo maana niliacha ghafla kuandika tena kwenye safu hii!
Sms hizo zilikuwa kali na ziliniumiza kwa sababu wakati huo zilipokuwa zikitumwa nilikuwa muda wote niko wodini hospitali ya KCMC, mjini Moshi, nikimuuguza baba!
Vyovyote vile, nimewasamehe. Maisha yanaendelea. Na kinachonifariji na kunipa nguvu za kuendelea kuandika ni yale maneno yaliyotamkwa na mwandishi maarufu wa vitabu wa zamani wa Marekani, Mark Twain, kwamba andika lakini usiogope shutuma au kulaniwa (write and be condemned).Nitaendelea kuandika kwa kuwa niko tayari kukosolewa, kushutumiwa na kulaaniwa. Hata hivyo, sina cha zaidi cha kuandika kuhusu Lowassa. Kuna wakati nilishawishika kumuandikia ‘tanzia ya kisiasa’ lakini nikaachana na wazo hilo kwa sababu ingekuwa sawa na kumchapa viboko farasi aliyekwishakufa (flogging a dead horse).
Labda tu niseme kwamba ilikuwa ni furaha iliyoje kwangu kwamba siku niliporejea Dar es Salaam kutoka kijijini ndiyo siku ambayo ilifahamika rasmi kwamba CCM imemkata Lowassa kuwania urais kwa sababu zile zile nilizozitaja kwenye ile makala yangu ya mwisho kwenye safu hii – kwamba Lowassa si msafi na si muumini wa ‘Janteloven’ (utamaduni wa kuuchukia ufisadi).
Kwa hakika, naipongeza Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM kwa kulikata mapema jina la Lowassa. Kwa kitendo chao hicho cha kijasiri, wametuma ujumbe kwa taifa zima kwamba pesa si kila kitu; kwamba ni ujinga kuruhusu matajiri kutuchagulia rais.
Hata hivyo, wakati nimefurahi mno na kukatwa kwa Edward Lowassa kuwania urais wa nchi yetu, sijasisimshwa na jina ambalo hatimaye CCM iliibuka nalo – jina la John Pombe Magufuli.
Kwa mtazamo wangu binafsi (si wa gazeti hili), John Pombe Magufuli, japo ni bora kuliko Lowassa, hawezi kuwa rais bora wa nchi yetu kama atashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Angefaa kuwa Waziri Mkuu kama akiwa na rais makini, mwenye busara na mchapakazi kama yeye lakini si yeye mwenyewe kuwa rais!
Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu John Pombe Magufuli ni mtu mwenye maamuzi ya pupa na ya jazba, na hivyo anahitaji mtu wa juu yake mwenye mamlaka zaidi wa kumdhibiti – na mtu huyo ni rais! Hebu fikiria mtu wa namna hiyo akiwa yeye mwenyewe ndiyo rais!
Hata kwenye zama zake za uwaziri, John Pombe Magufuli hakupata kunisisimua kuwa ni presidential material. Ili unielewe vyema, hebu rejea makala niliyoiandika kwenye toleo Na. 322, Oktoba 23, 2013 iliyokuwa na kichwa kinachosomeka: Magufuli ajiuzulu au ajifunze kufunga mdomo.
Nimekuwa nikifuatilia utendaji wake kwa muda mrefu, na nadiriki kusema kwamba John Pombe Magufuli ni mchapakazi hodari lakini mwenye kasoro kadhaa kubwa za kufanya maamuzi ya pupa, kuzomoka na kutoa kauli tata hadharani bila kwanza kupima athari zake. Kauli hizo ni kama ile ya kuwaambia wana Kigamboni wapige mbizi kama hawataki kulipa nauli mpya ya kivuko!
Ukiondoa kasoro hizo, ni kweli kwamba John Pombe Magufuli ni miongoni mwa mawaziri wachache katika Serikali ya Kikwete wanaochapa kazi. Yeye sheria ikishapitishwa husimama kidete kuitekeleza hadi nukta ya mwisho hata kama athari zake ni kubwa! Tena ataisimamia kwa ukali na vitisho.
Kwa hiyo, narudia kusisitiza kuwa, ukiondoa kasoro yake ya kuzomoka na kufanya maamuzi ya pupa bila kwanza kupima athari zake mbeleni, John Pombe Magufuli ni waziri mchapakazi.
Lakini, pamoja na uchapakazi wake huo, anavumilika kwenye uwaziri tu, na si kwenye urais. Kwenye urais hafai; maana anahitaji kufungwa ‘gavana’ na viongozi wengine wa juu zaidi yake yeye – yaani waziri mkuu au rais.
Uzoefu unaonyesha kwamba, wakati wa uwaziri wake, kazi hiyo ya kumfunga ‘gavana’ ilifanywa (si mara moja au mbili) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda au Rais Kikwete mwenyewe.
Si mara moja au mbili John Pombe Magufuli alidhalilishwa hadharani na wakubwa zake hao kwa sababu ya udhaifu wake huo wa maamuzi ya pupa na ya jazba. Hali hiyo ilisababisha heshima yake kwa umma ipungue, na hata kuonekana ukali na vitisho vyake ni vya chui wa karatasi (paper tiger)!
Labda nitoe mfano mmoja unaohusu suala lile alilolivalia njuga mwaka 2011 la bomoabomoa ya nyumba zilizowekwa “X” kwa kujengwa katika maeneo ya hifadhi ya barabara.
Itakumbukwa kwamba Magufuli aliielekeza Tanroads kupima barabara zote kuu nchini na kuwekea “X” nyumba zote zilizojengwa katika eneo la hifadhi ya barabara hizo.
Zoezi hilo la kitaifa lilitumia mamilioni ya fedha za walipakodi kulikamilisha.
Na lilipokaribia kukamilika ndipo John Pombe Magufuli akaanza vitisho vyake kwa wote ambao waliwekewa nyumba zao “X”.
Akawapa muda fulani wazibomoe wenyewe; vinginevyo zingebomolewa na matingatinga ya Tanroads bila ulipaji fidia. Waathirika wakaanza kulalamika na kutoa shutuma kibao kwa waziri huyo na serikali.
Rais Kikwete ndiye ‘aliyemfunga gavana’ John Pombe Magufuli asitekeleze zoezi hilo kwa ubabe – jambo ambalo bila shaka lingesababisha umwagaji damu na uvunjifu wa haki za binadamu.
Nakumbuka akiwa kule kwetu Mamba Miamba, wilayani Same, kufungua kituo (si kiwanda) cha tangawizi, Rais Kikwete alilalamikiwa na wanavijiji kuwa nyumba zao nyingi zimewekewa “X”, na kwamba Magufuli na Tanroads yake wamepania kuzivunja bila fidia.
Wanavijiji hao walilalamika kuwa wakati wakizijenga hapakuwa na alama yoyote kuonyesha kuwa ni eneo la hifadhi ya barabara, na pia walihoji serikali ilikuwa wapi wakati wanaanza kuzijenga mpaka wamemaliza, na wameishi humo kwa miaka mingi ndipo Serikali ijitokeze kuzibomoa?
Ni dhahiri wanavijiji walikuwa na hoja – hoja ambayo Magufuli hakuiona au aliamua tu kuipuuza. Hata hivyo, akijibu malalamiko yao hayo kwenye hotuba yake, Rais Kikwete aliwaambia wanavijiji hao kwamba wasiwe na hofu yoyote. Walale usingizi mnono na kwa amani kwa kuwa hakuna mtu atakayewabomolea nyumba zao.
Kuanzia hapo Magufuli akawa amefungwa ‘gavana’ na Kikwete kwenye suala hilo la bomoabomoa. Mpaka leo Magufuli hazungumzii tena zoezi la bomoabomoa.
Mfano mwingine wa pili ni wa tukio lile la mgomo ule wa wenye malori ya mizigo baada ya John Pombe Magufuli kuagiza watozwe asilimia tano kwa kila lori litakalozidisha uzito.
Wamiliki hao walikataa, na badala yake wakaamua kugoma. Wakati mgomo huo ukiendelea, John Pombe Magufuli, akitiwa nguvu na sheria kuhusu tozo hiyo mpya, akatamba lazima wenye malori walipe tozo hiyo, na kama hawataki, wayaondoe malori yao barabarani na kuyaegesha majumbani mwao!
Japo kweli tozo hiyo ipo kisheria, John Pombe Magufuli hakufikiria athari za kiuchumi kwa taifa kutekeleza agizo lake hilo kibabe.
Baada ya mgomo wa wenye malori kuendelea kwa siku kadhaa na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya pesa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akaingilia kati na kumpiga “stop” John Pombe Magufuli kwa kusitisha ulipaji wa tozo hiyo ya asilimia tano, na pia kuagiza pande mbili zikae chini kutafuta mwafaka - jambo ambalo Magufuli alilikataa mwanzoni.
Baada ya agizo hilo la Waziri Mkuu, mbwembwe, vitisho na jazba alizokuwanazo John Pombe Magufuli kuhusu tozo na mgomo huo wa wenye malori vikayeyuka haraka kama liyeyukavyo pande la barafu ukiliweka kwenye jua kali!
Huyo ndiye John Pombe Magufuli – mtu ambaye CCM imemuona ndiye anayefaa kuwa rais wetu mpya kuanzia Oktoba mwaka huu!
Na hapo, bado sijazungumzia kabisa mambo yake mengine yenye utata kama vile uamuzi wa kuuza nyumba za serikali na ule ya kukamata meli ya samaki ya kichina bila utafiti wa kutosha au hata suala la uwezo wake mdogo wa kuleta mageuzi ya maana (reforms) ndani ya CCM.
Hayo pengine si ya msingi kwa sasa kuyajadili. Swali la msingi la kujiuliza kwa sasa ni hili:Hivi John Pombe Magufuli akiwa rais, ni nani atakayethubutu kumfunga ‘gavana’ kwenye maamuzi yake ya pupa na ya kibabe kama Kikwete na Pinda walivyokuwa wakimfunga? Jibu mnalo wenyewe.
U-tingatinga wa Magufuli
Wakati Rais Kikwete akimtangaza rasmi John Pombe Magufuli pale Dodoma kuwa ndiye atakayebeba bendera ya CCM kwenye mbio za kuusaka urais alimwita kuwa ni “tingatinga” yaani kwa Kiingereza bulldozer.
Sijui Kikwete alifikiria nini kumwita vile hadharani. Tujuavyo sote, bulldozer ni mashine kubwa inayosambaza udongo na kusawazisha ardhi kwa kufagia kila kilicho mbele yake. Siamini, hivyo basi, kuwa ni sifa kuitwa bulldozer. Kumwita mtu bulldozer ni sawa na kumwita mbabe.
Hivi kweli tunahitaji bulldozer ndiye awe rais wetu na si mtu mwenye hekima, busara, na mfikiriaji mwenye maono (vision)? Hivi kweli tumefika mahali u-bulldozer nao umekuwa ni sifa ya urais?
Ni nani sasa atamfunga ‘gavana’ bulldozer John Pombe Magufuli kama kweli atafanikiwa kuwa rais wetu mpya Oktoba mwaka huu?
Ndugu zangu, nihitimishe kwa kusema hivi: ni kweli kwamba ili kuinyoosha nchi hii anahitajika rais ambaye, kwa kiasi fulani ni ‘dikteta poa’ (benevolent dictator), lakini kwa mtu huyu - bulldozer John Pombe Magufuli napata hisia kuwa atakuwa zaidi ya ‘dikteta poa’.
Kama John Pombe Magufuli ni huyuhuyu tunayemjua sote, tusitaraji mapya kutoka kwake zaidi ya vitisho, ubabe na maamuzi ya jazba.
Uchapakazi unaoandamana na kasoro hizo kubwa, licha ya uhodari wake wa kukariri kilomita za barabara zilizojengwa na zinazojengwa, havitoshi kumfanya bulldozer John Pombe Magufuli awe rais bora.
Itabidi ‘azaliwe upya’ kama anataka kuwa rais mzuri wa tano wa Tanzania. Anaweza ‘kuzaliwa upya’?
Tafakari.
*Toleo lijalo: Kwa nini Slaa (Chadema) ndiye afaaye kumkabili Magufuli.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kama-akiwa-rais-nani-atamfunga-%E2%80%98gavana%E2%80%99-magufuli#sthash.YvQeMABe.dpuf

No comments :

Post a Comment