dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 10, 2015

Mbowe: Kwa nini Lowassa, si Dk Slaa

Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akihutubia wananchi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mbowe, mjini Karatu, mkoani Arusha jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
By Waandishi Wetu, Mwanachi
Karatu/Moshi. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana alitua kwa mara ya kwanza kwenye Jimbo la Karatu ambako Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi sababu za kumuacha Dk Willibrod Slaa kugombea urais na badala yake kumteua waziri huyo mkuu wa zamani.
Lowassa pia alivuta watu wengi kwenye mkutano uliofanyika Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi, ambako Jaji Salma Maghembe alilazimika kuahirisha kwa muda kutoa uamuzi wa ubishani wa kisheria katika kesi ya mauaji ya bilionea maarufu, Erasto Msuya kutokana na kelele zilizosababishwa na honi za pikipiki, vuvuzela na nyimbo. Mahakama hiyo inapakana na Uwanja wa Mashujaa.
Kwenye mkutano wa kampeni za urais uliofanyika Karatu, Mbowe alilazimika kuzungumzia suala la Dk Slaa, ambaye alijivua wadhifa wake akipingana na viongozi wenzake katika taratibu za kumpokea Lowassa kutoka CCM na kumpa fursa ya kugombea urais.
Akizungumza kabla ya kumpisha Lowassa ahutubie, Mbowe alisema malengo ya nchi ni makubwa kuliko Dk Slaa na Lowassa.
Alisema Chadema iko tayari kumsamehe Dk Slaa kwa kuwa kila mtu kuna wakati hufanya makosa ambayo ni vitu vinavyosameheka.
“Nasikitika kwamba tumepoteza askari mmoja, lakini mapambano ya kuikomboa nchi yanaendelea,” alisema Mbowe ambaye alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza na wananchi wa Karatu tangu Dk Slaa alipojiondoa Chadema mapema mwezi uliopita.
“Mwaka 2010 niliombwa kugombea urais, lakini nilimshawishi Dk Slaa agombee akaniuliza, “mwenyekiti nitaweza?” Nikamjibu, “utaweza”, kwa kuwa nilimpima na alikuwa na sifa na uwezo wa kuwa rais,” alisema Mbowe.
“Mwaka huohuo, rafiki yangu alianza mahusiano ya kifamilia. Dokta wetu akawa siyo yule tuliyemzoea. Ilipofika mwaka 2014 akaniambia niwe mgombea, lakini nikamwambia bado anafaa hivyo nikapeleka mapendekezo kwenye vikao vya chama wakaniambia, ‘mwenyekiti kwa nini unaleta mapendekezo?’ Nikawaambia ndani ya Chadema hatugombanii uongozi.
“Tulimpendekeza Dk Slaa agombee urais. Chama hiki tumekijenga kisayansi tukafanya utafiti kwa kutumia watafiti kutoka nje ambao hawamjui Lowassa. Mbowe wala Slaa. Maswali yetu yalikuwa manne; la kwanza nini matumaini ya Chadema kukamata nchi chini ya Dk Slaa? Nani miongoni mwa wana-CCM anaweza kuongoza mabadiliko? Tufanye nini ili safari yetu iwe ya uhakika? Lakini majibu hayakuwa mazuri.”
Alisema watafiti hao waliwaambia Chadema ina nguvu lakini ifanye jitihada iipasue CCM ili iweze kufika na iliwaeleza kuwa atakayekisumbua chama hicho kikuu cha upinzani ni Lowassa kwa kuwa ana kundi kubwa ndani na nje ya CCM.
Mbowe alisema kuwa baada ya kupata majibu hayo, Dk Slaa akamwambia wafanye njia gani ili waweze kumpata Lowassa, lakini yeye Mbowe akamwambia amuachie suala hilo.
Katika mkutano huo mbali na Mbowe, Lowassa aliambatana na mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale-Mwiru na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Akizungumza katika mkutano huo, Kingunge aliwaambia wananchi hao kwamba CCM siyo chama ambacho kinaweza kuleta mabadiliko kwa kuwa kimeishiwa pumzi hivyo hakiwezi kupanda mlima wa mabadiliko.
Kwa upande wake, Lowassa alisema katika historia ya Karatu, haijawahi kutokea watu wengi kiasi hicho hivyo akawaomba kura ili aweze kuwasaidia kuleta mabadiliko.
Awali, akiwa katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Komboko, Siha mkoani Kilimanjaro, Lowassa aliwaambia wananchi kuwa amedhamiria kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali nchini hivyo anahitaji wampe kura za kutosha.
Mjini Moshi, mitaa na vitongoji vyake ilijaa shangwe kwa takriban saa nane kuanzia saa mbili asubuhi wakati wakazi wakimsubiri Lowassa. Wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wakazi wengine wa mjini hapa, wakiwa na pikipiki na magari, walikuwa wakizunguka mitaa mbalimbali wakihanikiza kwa honi na tarumbeta aina ya vuvuzela kusubiri mkutano uliofanyika Uwanja wa Mashujaa.
Hekaheka hizo ziliathiri pia usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya bilionea Msuya na kusababisha Jaji Maghembe kuahirisha kutoa uamuzi mdogo wa mabishano ya kisheria yaliyoibuka kati ya mawakili wa utetezi na wale wanaoendesha kesi hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe, alisema CCM haiwezi kubadilika na kuongoza mabadiliko.
“Naomba kuwatahadharisha wananchi wa Moshi kuwa CCM ni ileile, Magufuli ni yuleyule. Magufuli na CCM ni pete na kidole,” alisema Mbowe.
“Magufuli anasema Serikali ya Magufuli itakuwa ni ya viwanda, tunamuuliza aliyeua viwanda vya Moshi, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam ni CCM au ni Chadema?”aliuliza na kujibiwa “ni CCM.”
Kingunge, aliyejivua uanachama wa CCM mwishoni mwa wiki, alisema tatizo la ajira kwa Watanzania limeshindwa kutatuliwa na CCM kutokana na uongozi mbovu.
Alisema ni Lowassa pekee na Serikali atakayoiunda ndiyo ambao wanaweza kutoa suluhusho la ajira na matatizo mengi ya Watanzania.
Katika mkutano huo, aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Lameck Kaaya na Diwani wa Kata ya Kilimanjaro kwa tiketi ya CCM (2005-2010), alijiunga na Chadema.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment