dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, April 23, 2018

CAG abaini Bado kuna matatizo mkataba wa Mlimani City!

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini bado kuna matatizo katika utekelezaji wa mkataba tata kati ya serikali na mwekezaji wa mradi wa Mlimani City.Katika ripoti yake ya mwaka 2015/16, CAG Prof. Mussa Juma Assad, alibainisha kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika mkataba huo ikiwa ni pamoja na rasilimali zilizopo kutojulikana zitakuwa mali ya upande upi baada ya kufika ukomo wa muda wa mwekezaji.

Kwenye ripoti yake ya mwaka 2016/17 kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma, CAG anabainisha kuwa baadhi ya mapendekezo yake ya mwaka uliotangulia hayajafanyiwa kazi na wahusika.

Anasema amebaini kuna ucheleweshwaji wa utekelezaji na ukamilikaji wa baadhi ya miradi ambayo menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliishauri kuuangalia upya mkataba ilioingia na kampuni ya Mlimani City Holding (MHL) ili kuharakisha umaliziaji wa miradi.

Prof. Assad anaeleza kuwa majibu aliyopewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu suala hilo ni kwamba tarehe iliyopangwa ya kukamilisha mradi ilisogezwa kupitia mkataba wa utendaji kutoka Septemba Mosi, 2006 hadi Desemba 31, 2019.

“Wakati wa mkutano wa pamoja uliofanyika Aprili 20, 2017, kati ya UDSM, Kituo cha Uwekezaji (TIC) na MHL, kampuni hiyo ilisema kuwa wanataka kuweka bustani ya mimea (botanical garden) kabla ya mwisho ya kipindi cha maendelezo lakini hakuna mipango ya kujenga hoteli ya nyota nne,” CAG Assad anaeleza katika ripoti yake hiyo iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.

Hata hivyo, anaeleza kuwa UDSM na TIC walimwomba MHL kutafakari upya juu ya hoteli kulingana na mkataba uliopo na MHL aliahidi kufanya hivyo.

Anasema UDSM tayari imeanzisha mchakato wa kupitia upya mkataba wa kukodisha ardhi (Ground Lease Agreement) na kwamba suala hilo ameona lipo katika hatua za utekelezaji na atafuatilia utekelezaji wake kamili.

Kutokana na ukiukwaji wa malipo ya kodi ya UDSM alioubaini katika ukaguzi wake, CAG Assad anaishauri menejimenti ya chuo kufanya upya hesabu za gawiwo lake la asilimia 10 kutokana na mkataba na kuomba kulipwa na mpangaji kiasi kilichokuwa kimekosewa.

Pia anaishauri kuuwasiliana na mpangaji na kufikiria kubadilisha mkataba ili kuweka vifungu ambavyo vitaruhusu Idara ya Ukaguzi ya Ndani ya chuo kuangalia mapato na gharama za uendeshaji za mradi.

Prof. Assad anabainisha kuwa, amepokea maelezo ya Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu suala kwamba menejimenti imeyapokea mapendekezo na hatua stahiki zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutengeneza ankara za ada iliyokuwa imekosewa ikifuatiwa na ripoti ya mahitaji ya malipo ya tofauti kati ya jumla kuu na kiasi kilichokwishalipwa chuoni (UDSM).

CAG pia anasema UDSM inafuatilia mambo yanayohusiana na MHL ili kuanzisha njia bora ambayo itakuwa na manufaa ya pamoja na kiwango kikubwa cha kukubalika katika mkataba ambao ni hati inayoongoza kazi pande zote mbili kuhusiana na mradi wa Mlimani City.

Anasema anafuatilia utekelezaji wa suala hilo pamoja na udhaifu wa ufuatiliaji na usimamizi wa mapato kutoka kwa wapangaji wadogo.

Anaishauri menejimenti ya chuo kutekeleza vifungu na vipengele vyote vya hati ya makubaliano ya upangaji kikiwamo kifungu 11.2(l) cha hati ya makubaliano ambacho kinakitaka chuo kuwathibitisha wapangaji wadogowadogo.

Prof. Assad anasema majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu udhaifu huo ni kwamba UDSM inapaswa kuidhinisha wapangaji kabla ya makubaliano rasmi ya kukodisha na kusainiwa ili kuongeza uwazi juu ya makubaliano ya kimkataba. “Hadi sasa, UDSM imeimarisha mahitaji haya ya kiutaratibu. Nitafuatilia utekelezaji wake kamili,” anasema.

Prof. Assad pia anasema amebaini kukosekana kwa haki ya UDSM kujua kazi zinazofanywa na MHL, akikishauri chuo hicho kuwasiliana na kampuni hiyo ili kupata haki ya kukagua shughuli za miradi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Anasema majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu suala hilo ni kwamba Ofisa Uhusiano wa UDSM ameshahakiki taarifa zote na kwamba sasa hakuna kizuizi cha MHL, lakini atafuatilia utekelezaji wake kamili.

No comments :

Post a Comment